KANUNI ZA UFUGAJI BORA WA MBUZI NA KONDOO
Mbuzi na kondoo wanaweza kufugwa kwa gharama nafuu na
kuishi katika mazingira magumu kama ya maradhi na ukame ikilinganishwa na
ng’ombe. Kutokana na umbile lao dogo wanaweza kufugwa katika eneo dogo na pia
wanaweza kuhudumiwa na familia yenye nguvukazi na kipato kidogo. Uzao wa muda
mfupi unamwezesha mfugaji kupata mbuzi/kondoo wengi kwa kipindi kifupi. Wanyama
hao hufugwa kwa ajili ya nyama, maziwa, ngozi, sufu na mazao mengine kwa
matumizi ya familia na kuongeza kipato. Ufugaji bora wa mbuzi na kondoo
uzingatie kanuni zifuatazo:-
i) Wafugwe kwenye banda
au zizi bora, ii) Wachaguliwe kutokana
na sifa za koo/aina na lengo la uzalishaji (nyama, maziwa au sufu), iii)
Wapatiwe lishe sahihi kulingana na umri na mahitaji ya mwili, iv) Kuzingatia
mbinu za kudhibiti magonjwa kama inavyoshauriwa na mtaalam wa mifugo, v) Kuweka
na kutunza kumbukumbu sahihi za uzalishaji; na vi) Kuzalisha nyama, maziwa au
sufu yenye ubora unaokidhi mahitaji ya soko
K o n d o o / M b u zi
Zizi au Banda la Mbuzi/Kondoo Mbuzi/kondoo wanaweza
kufugwa katika mifumo ya huria, shadidi na kwa kutumia njia zote mbili. Zizi
hutumika katika mfumo huria ambapo mbuzi/kondoo huchungwa wakati wa mchana na
kurejeshwa zizini wakati wa usiku. Zizi bora ni lile lenye sifa zifuatazo:-
• Lililo imara
linaloweza kumkinga mbuzi/kondoo dhidi ya wanyama hatari na wezi,
• Lililojengwa mahali pa mwinuko pasiporuhusu
maji kutuama,
• Ukubwa wa zizi uzingatie
idadi na umri wa mifugo. Ni vema mbuzi/kondoo watengwe kulingana na umri wao;
na
• Liruhusu usafi
kufanyika kwa urahisi.
Pale ambapo
mbuzi/kondoo wanafugwa kwa mfumo wa shadidi hufugwa katika banda wakati wote.
Banda bora la mbuzi/kondoo linatakiwa kuwa na sifa zifuatazo:-
• Imara, lenye uwezo wa kuwahifadhi kiafya na
pia dhidi ya hali ya hewa hatarishi kwa mfano jua kali, upepo, baridi na mvua
pamoja na wanyama hatari,
• Lenye mwanga, hewa na
nafasi ya kutosha inayoruhusu usafi kufanyika kwa urahisi,
• Lijengwe sehemu
isiyoruhusu maji kutuama na liwe mbali kidogo na nyumba ya kuishi watu. Pia
ujenzi uzingatie mwelekeo wa upepo ili hewa kutoka bandani isiende kwenye
makazi,
• Liwe na sakafu ya
kichanja chenye urefu wa mita 1 kutoka ardhini (Kwa banda la mbuzi),
• Liwe na sehemu ya
kuwekea chakula, maji na mahali pa kuweka jiwe la chumvichumvi; na
• Liwe na vyumba
tofauti kwa ajili ya majike na vitoto, mbuzi/kondoo wanaokua, wanaonenepeshwa
na wanaougua.
Vifaa vya Kujengea na Vipimo vya Banda Inashauriwa banda
la mbuzi/kondoo lijengwe kwa kutumia vifaa vinavyopatikana kwa urahisi katika
eneo husika. Ukubwa wa banda utategemea idadi ya mbuzi/kondoo wanaofugwa humo
na ukubwa wa umbo.
Eneo la mbuzi/kondoo linalotakiwa Kundi la Mbuzi/Kondoo Eneo kwa Mnyama Mmoja (Mita2), Vitoto 0.3,
Wasio na mimba 1.5, Wenye mimba 1.9 na
Dume 2.8
• Paa lijengwe kwa
kutumia vifaa kama miti, mbao, na kuezekwa kwa nyasi, makuti, majani ya
migomba, mabati au hata vigae kwa kutegemea uwezo wa mfugaji,
• Kuta zijengwe kwa
kutumia mabanzi, mbao, nguzo, wavu wa waya, fito na matofali. Kuta ziwe imara
zinazoruhusu hewa na mwanga wa kutosha. Mlango uwe na ukubwa wa sentimita 60 x
150,
• Sakafu inaweza kuwa
ya udongo au zege. Sakafu ya kichanja inaweza kujengwa kwa kutumia miti, fito,
mianzi, mbao au mabanzi na iweze kuruhusu kinyesi na mkojo kupita. Chumba cha
majike na vitoto kiwe na nafasi ya sentimita 1.25 kati ya papi na papi, fito na
fito au mti hadi mti. Chumba cha mbuzi/kondoo wakubwa iwe sentimita 1.9 kati ya
mbao na mbao.
Uchaguzi wa Mbuzi/Kondoo wa Kufuga Madhumuni ya kuchagua
mbuzi au kondoo wa kufuga ni kuboresha uzalishaji na kuendeleza kizazi bora.
Kuna aina nyingi za mbuzi/kondoo wanaoweza kufugwa kulingana na mazingira na
mahitaji ya mfugaji. Uchaguzi hufanyika kwa kuangalia umbile, uzalishaji na
kumbukumbu za wazazi kama vile umbo kubwa, ukuaji wa haraka, uwezo wa kutunza
vitoto na kutoa maziwa mengi. Mbuzi wanaofaa kwa ajili ya maziwa ni aina ya
Saanen, Norwegian na Toggenburg pamoja na chotara wao.
Mbuzi wanaofaa kwa
ajili ya nyama ni Boer na chotara wao, mbuzi wa
asili kama vile Pare white , Newala na Ujiji.
Mbuzi aina ya Malya ( Blended ) wanafaa kwa
ajili ya nyama na maziwa.
Aidha, kondoo aina ya Black Head
Persian (BHP), Masai red , Suffolk na Hampshire wanafaa
kufugwa kwa ajili ya nyama. Merino na Lincoln hufugwa kwa ajili ya sufu, wakati Corriedale
na Romney hufugwa kwa ajili ya nyama na sufu. Hapa Tanzania kondoo
wanaopatikana kwa wingi ni Black Head Persian , Masai Red Dopper na kondoo wengine wa asili.
Mbuzi/kondoo jike wanaofaa kwa ajili ya kuzalisha maziwa na nyama
wawe na sifa zifuatazo:-
• Historia ya kukua
upesi, kuzaa (ikiwezekana mapacha) na kutunza vitoto vizuri, • Umbo la mstatili
linaloashiria utoaji wa nyama nyingi; na
• Asiwe na ulemavu wa
aina yoyote
Sifa za Ziada kwa Mbuzi wa Maziwa
• Awe na miguu ya nyuma
iliyo imara na iliyonyooka na yenye nafasi kwa ajili ya kiwele; na
• Awe na kiwele kikubwa
na chuchu ndefu zilizokaa vizuri
Sifa za Dume Dume bora
awe na sifa zifuatazo:-
• Miguu iliyonyooka,
imara na yenye nguvu,
• Asiwe na ulemavu wa
aina yoyote,
• Mwenye uwezo na nguvu
ya kupanda; na
• Mwenye kokwa mbili
zilizo kaa vizuri na zinazolingana Angalizo: Dume lichaguliwe kwa makini kwa
sababu “dume ni nusu ya kundi”.
Utunzaji wa Vitoto vya Mbuzi/Kondoo Utunzaji huanza mara tu baada ya
kuzaliwa. Mfugaji ahakikishe:-
• Kitoto cha mbuzi/kondoo kinapata maziwa ya
mwanzo (dang’a) ndani ya masaa 24 tangu kuzaliwa na kwa muda wa siku 3,
• Kama kinanyweshwa maziwa, kipewe lita 0.7-
0.9 kwa siku. Maziwa haya, ni muhimu kwani yana viinilishe na kinga dhidi ya
magonjwa,
• Iwapo mama hatoi
maziwa au amekufa, inashauriwa kutengeneza dang’a mbadala au kama kuna
mbuzi/kondoo mwingine aliyezaa anaweza kusaidia kukinyonyesha kitoto hicho,
• Kitoto cha
mbuzi/kondoo kiendelee kunyonya kwa wiki 12 - 16. Wiki 2 baada ya kuzaliwa,
pamoja na maziwa, kianze kupewa vyakula vingine kama nyasi laini na chakula cha
ziada ili kusaidia kukua kwa tumbo. Aidha, kipewe maji wakati wote,
• Vyombo vinavyotumika
kulishia vinakuwa safi muda wote,
• Kitoto cha
mbuzi/kondoo kiachishwe kunyonya kikiwa na umri wa miezi 3 hadi 4 kutegemea
afya yake; na
• Vitoto vipatiwe kinga
na tiba ya magonjwa kulingana na ushauri wa mtaalam wa mifugo.
Matunzo Mengine Utambuzi Mbuzi huwekewa alama ili
atambulike kwa urahisi na kuwezesha utunzaji wa kumbukumbu zake. Shughuli hii
hufanyika kwa mbuzi/kondoo akiwa na umri wa siku 3 - 14. Njia zitumikazo ni
pamoja na:
• Kuweka alama sikioni
kwa kukata sehemu ndogo ya sikio,
• Kumpa jina kwa
wafugaji wenye mbuzi wachache,
• Kumvisha hereni ya
chuma au plastiki yenye namba kwenye sikio,
• Kumvalisha mkanda
wenye namba shingoni; na
• Kuweka namba kwa
kuunguza sehemu ya ngozi ya mbuzi. Pale mfugaji anapotumia njia hii inashauriwa
aweke alama kwenye eneo ambalo halitaathiri ubora wa ngozi
Kuondoa vishina vya
pembe Mbuzi/kondoo aondolewe vishina vya pembe akiwa na umri kati ya siku 3
hadi 14. Visipoondelewa hukua na kusababisha kuumizana na kuhitaji nafasi kubwa
kwenye banda. Kazi hii ifanywe na mtaalam wa mifugo.
Kuhasi Vitoto vya
mbuzi/kondoo ambavyo havitatumika kwa ajili ya kuendeleza kizazi vihasiwe kabla
ya kufikia umri wa miezi 3. Kazi hii ifanywe na mtaalam wa mifugo.
Utunzaji wa Mbuzi/Kondoo wa Miezi 4 - 8 Mbuzi wa miezi 4
mpaka 8 ni wale ambao wameacha kunyonya mpaka umri wa kupandishwa kwa mara ya
kwanza. Mbuzi wa umri huu wana uwezo wa kula aina mbalimbali za malisho kama
nyasi, mikunde, miti malisho na mabaki ya mazao wakati kondoo hupendelea zaidi
nyasi fupi. Wakati wa kiangazi huhitaji kupatiwa chakula cha ziada au kupewa
pumba za nafaka mbalimbali, mashudu ya alizeti, pamba na dengu, majani ya
mikunde yaliyokaushwa, madini na vitamini.
Katika ufugaji huria ni
vema kuzingatia idadi ya mbuzi/kondoo inayoweza kuchungwa katika eneo, aina na
hali ya malisho.
Ili mbuzi/kondoo aweze
kukua na kufikia uzito wa kuchinjwa/kupevuka mapema, mfugaji anapaswa kufuata
kanuni za ufugaji bora zifuatazo:-
• Kumpatia vyakula vya
ziada kwa muda wa miezi 2 mfululizo kiasi cha kilo 0.2 – 0.7 kwa siku kuanzia
anapoachishwa kunyonya,
• Kumpatia dawa ya
kuzuia minyoo kila baada ya miezi 3 na kutoa kinga za magonjwa mengine kama
itakavyoshauriwa na mtaalam wa mifugo,
Zingatia kanuni za
ufugaji bora ili ku jihakikishia usalama wa chakula na kujiongezea kipato
• Kuchanja na kuogesha
ili kuzuia magonjwa mbalimbali,
• Kukata kwato mara
zinapokuwa ndefu; na
• Kuhasi madume
yasiyotumika kuzalisha.
Umri wa Kupandisha
Mbuzi/Kondoo Mbuzi/kondoo wakitunzwa vizuri
wanaweza kupandishwa wakiwa na umri wa miezi 8 hadi 12 kwa mbuzi/kondoo
walioboreshwa na miezi 18 hadi 24 kwa mbuzi wa asili kutegemea afya yake. Hata
hivyo, inashauriwa wapandishwe wanapofikia uzito wa kilo 12 au zaidi na
wasipandishwe mbuzi/kondoo wa ukoo mmoja.
Dalili za joto Mfugaji anashauriwa asimpandishe jike
kabla hajafikisha umri wa kupandwa wa miezi 8 hadi 12 kwa mbuzi/kondoo
walioboreshwa na miezi 18 hadi 24 kwa mbuzi wa asili hata kama ataonyesha
dalili ya kuhitaji dume. Mbuzi/kondoo aliyezaa anaweza kupandishwa siku 30-60
baada ya kuzaa. Mbuzi/kondoo aliyeko kwenye joto huonyesha dalili zifuatazo:-
• Hutingisha/huchezesha
mkia,
• Hupanda na kukubali
kupandwa na wengine,
• Hutoa ute mweupe
ukeni,
• Huhangaika mara kwa
mara na kupiga kelele,
• Hufuata madume,
• Hamu ya kula
hupungua,
• Hukojoa mara kwa
mara,
• Uke huvimba na huwa
mwekundu kuliko ilivyo kawaida; na
• Kwa mbuzi
anayekamuliwa hupunguza kiwango cha maziwa
Mbuzi/kondoo apelekwe
kwa dume mara tu dalili za joto zinapoonekana kwani joto hudumu kwa wastani wa
siku 2 (saa 48). Chunguza tena dalili za joto baada ya siku 19 hadi 21 na kama
dalili hazitaonekana tena kuna uwezekano mkubwa
Zingatia kanuni za
ufugaji bora ili ku jihakikishia usalama wa chakula na kujiongezea kipato
kuwa mbuzi/kondoo
amepata mimba. Mfugaji apange msimu mzuri wa mbuzi/kondoo kuzaa. Msimu mzuri ni
mara baada ya mvua.
Utunzaji wa Mbuzi/Kondoo Mwenye Mimba Kwa kawaida
mbuzi/kondoo hubeba mimba kwa muda wa miezi 5. Utunzaji wa mbuzi/kondoo mwenye
mimba ni muhimu kwani ndiyo chanzo cha kupata vitoto vyenye afya bora. Mfugaji
anashauriwa kufuata kanuni zifuatazo: • Apatiwe vyakula vya ziada kilo 0.2 –
0.7 kwa siku ili kutosheleza mahitaji yake na kitoto kinachokua tumboni, •
Apatiwe nyasi, miti malisho na mikunde mchanganyiko kilo 1.8 – 2.5 kwa siku.
Dalili za Mbuzi/Kondoo Anayekaribia Kuzaa
• Huhangaika kwa kulala
na kuamka mara kwa mara,
• Sehemu ya nje ya uke
hulegea,
• Hujitenga na kundi na
hutafuta sehemu kavu na yenye kivuli,
• Hupiga kelele; na
• Hutokwa na ute mzito
ukeni. Mfugaji akiona dalili hizi anashauriwa asimruhusu mbuzi/kondoo kwenda
machungani, bali amtenge kwenye chumba maalum, ampatie maji ya kutosha na
kumuandalia sehemu ya kuzalia.
Utunzaji wa
Mbuzi/Kondoo Anayenyonyesha Mbuzi/kondoo anayenyonyesha huhitaji chakula kingi
zaidi ili kukidhi mahitaji ya mwili na kuzalisha maziwa kwa ajili ya
kitoto/vitoto. Pamoja na nyasi, mikunde na majani ya miti malisho kilo 1.8 –
2.5 kwa siku ni muhimu apewe chakula cha nyongeza kilo 0.3 – 0.8 kwa kila lita
ya maziwa inayoongezeka baada ya lita 2 na maji safi, salama na ya kutosha
wakati wote.
Taratibu za Kuzingatia Katika Ukamuaji wa Mbuzi wa Maziwa
Lengo la ufugaji wa
mbuzi/kondoo wa maziwa ni kupata maziwa mengi, safi na salama pamoja na mazao
yatokanayo na maziwa. Mambo muhimu ya kuzingatia ni:-
• Sehemu ya kukamulia
iwe safi na yenye utulivu,
• Mbuzi/kondoo awe na
afya nzuri, msafi, na kiwele kioshwe kwa maji safi ya uvuguvugu,
• Mkamuaji
asibadilishwe badilishwe awe msafi, mwenye kucha fupi na asiwe na magonjwa ya
kuambukiza,
• Vyombo vya kukamulia
viwe safi; na
• Maziwa ya mwanzo
kutoka kila chuchu yakamuliwe kwenye chombo maalum (strip cup) ili kuchunguza
ugonjwa wa kiwele.
Utunzaji wa Dume Bora la Mbegu Dume bora la mbegu ni
muhimu litunzwe ili liwe na uwezo wa kutoa mbegu bora, kupanda na kuzalisha.
Dume bora huanza kupanda akiwa na umri kati ya miezi.8 - 10 kwa mbuzi
walioboreshwa. Katika msimu wa kupandisha dume moja liruhusiwe kupanda majike
40 hadi 50. Aidha, inashauriwa madume wenye umri wa miezi 8 – 9 waruhusiwe
kupanda majike ambao ndio mara ya kwanza kupandwa.
Dume apatiwe:-
• Malisho ya kutosha na
vyakula vya ziada kiasi kisichopungua kilo 0.2 – 0.7 kwa siku na maji ya
kutosha, • Majani ya miti malisho, mikunde na nyasi mchanganyiko na mabaki ya
mazao; na
• Kilo 0.45 hadi 0.9 za
chakula cha ziada za nyongeza kwa siku kulingana na uzito wake na wingi wa
majike anayopanda.wiki 2 kabla na baada ya kuanza kupanda.
Matunzo Mengine Kukata Mkia
Mara nyingine kondoo
hukatwa mkia ili kuruhusu mtawanyiko mzuri wa mafuta katika misuli mwilini. Pia
kondoo aliyekatwa mkia huwa msafi. Kazi hii ifanywe kama itakavyoshauriwa na
mtaalam wa mifugo kwa kutumia vyombo maalum. Inashauriwa mkia ukatwe urefu wa
sentimita 2.5 – 3.8 kutoka kwenye shina la mkia wakati kondoo akiwa na umri wa
siku 3 mpaka mwezi 1.
Kumnyoa Kondoo wa Sufu
Sufu hunyolewa wakati kondoo akiwa hai au amechinjwa. Kwa kawaida hunyolewa miezi 6 hadi mwaka 1
ambapo sufu huwa imefikia urefu wa sentimita 15 – 20. Vifaa vinavyotumika ni
pamoja na mikasi au visu maalum. Uangalifu unahitajika wakati wa kunyoa ili
ngozi ya kondoo isiharibike. Unyoaji ufanyike wakati wa kiangazi na siyo wakati
wa mvua, kondoo akiwa na mimba au kipindi cha majani kutoa mbegu.
Udhibiti wa Magonjwa ya Mbuzi na Kondoo Magonjwa
husababishwa na vimelea jamii ya virusi, bakteria, protozoa na riketsia.
Magonjwa mengine husababishwa na upungufu wa viinilishe, vitamini na protini.
Dalili za mbuzi/kondoo mgonjwa ni pamoja na:- ¾ Manyoya husimama, ¾ Kuzubaa,
kusinzia, kukohoa na kupiga chafya, ¾ Kukosa hamu ya kula na kunywa maji, ¾
Kujitenga na kundi, ¾ Kuvimba taya la chini, ¾ Kupumua kwa shida, ¾ Kutokwa na
machozi na makamasi, ¾ Kuwa na upele au uvimbe kwenye sehemu ya mwili; na ¾
Kutupa mimba.
• Hatua za haraka za
kumuona mtaalamu wa mifugo zichukuliwe iwapo baadhi ya dalili hizi zitaonekana,
• Mbuzi na kondoo
wachanjwe dhidi ya magonjwa ya homa ya maapafu. Ugonjwa huu ni hatari sana na
huenea kwa njia ya hewa na unaweza kusababisha vifo kati ya asilimia 60-100,
• Kila baada ya miezi 6
mifugo ipatiwe kinga dhidi ya ugonjwa wa miguu na midomo na magonjwa mengine
kama Kimeta, bonde la ufa, kutupa mimba na chambavu (BQ) zitolewe kulingana na
ushauri wa mtalaam wa mifugo,
• Kama kuna wanyama
walioathirika watengwe kwenye kundi, wasisafirishwe au kuuzwa,
• Mbuzi/kondoo wapatiwe
dawa ya minyoo. Vitoto vya mbuzi/kondoo vipatiwe dawa ya minyoo vinapofikia
umri wa mwezi 1. viendelee kupatiwa dawa ya minyoo kila mwezi hadi vinapofikia
miezi 5 na baada ya hapo vipatiwe dawa ya minyoo kila baada ya miezi 3 - 4; na
• Zingatia usafi wa
banda ili kuwakinga na ugonjwa wa kuharisha na kuharisha damu na magonjwa
mbalimbali.
Picha ya banda la mbuzi
Picha ya banda la mbuzi
Utunzaji wa kumbukumbu
Utunzaji wa Kumbukumbu za Mifugo Kuweka kumbukumbu za
mifugo ni muhimu katika uzalishaji kwa ajili ya kutambua kosaafu, gharama za
utunzaji na faida. Pia, humsadia mfugaji kufanya maamuzi katika uendelezaji wa ufugaji wake.
Mtalaamu wa mifugo pia anaweza kutumia kumbukumbu hizi ili kumsaidia mfugaji
kuboresha ufugaji wake. Kumbukumbu muhimu zinazohitajika kutunzwa ni:-
• Kumbukumbu za idadi
na ukuaji wa wanyama waliopo, jinsi zao, uzito wa mbuzi/kondoo kwa kila mwezi
ili kufuatilia ukuaji wake, tarehe ya kuachishwa kunyonya na idadi ya
waliouzwa,
• Kumbukumbu ya uzazi
zinazoonyesha tarehe ya kuzaliwa, namba yake, jinsi yake, aina (breed), namba
ya dume/jike, na uzito wa kuzaliwa,
•Kumbukumbu za
upandishaji zinazoonyesha namba ya mbuzi/kondoo anayepandwa, tarehe ya joto na
ya kupandwa, namba ya dume lililotumika kupanda, tarehe ya joto la pili kama
atarudia na tarehe ya kuzaa,
• Kumbukumbu za chanjo
na matibabu zinazoonyesha namba ya mbuzi/kondoo, tarehe ya matibabu, aina ya
chanjo au ugonjwa, dawa iliyotumika, idadi ya waliokufa na waliopona na jina la
mtaalam aliyetibu,
• Kumbukumbu za maziwa
zinazoonyesha namba ya mbuzi/kondoo, tarehe ya kuzaa, kiasi cha maziwa kwa
siku, na kiasi cha maziwa kwa kipindi chote cha kukamuliwa, tarehe ya kuacha
kukamua na idadi ya siku alizokamuliwa,
• Kumbukumbu za mapato
na matumizi zinazoonyesha mapato na matumizi, vitu vilivyouzwa au kununuliwa
kwa siku, kiasi cha fedha unachokuwa nacho kila wakati, kiasi cha fedha
unachodai na kudaiwa.
cyprianoanimalfarms .blogspot.com
No comments:
Write comments